Wanafunzi wa shule za sekondari wakiwa katika midahalo yenye lengo la kupanua uelewa wao
MPANGO wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari nchini (MMES) uliolenga kila kata nchini kuwa na shule ya sekondari, umefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Umewezesha wanafunzi wengi kupata nafasi za kujiunga na masomo hayo.
Kufanikiwa huko, kunaleta matumaini kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo, nchi itakuwa na wasomi wengi waliohitimu elimu ya sekondari, ukilinganisha na miaka mingi iliyopita, kabla ya mpango huo haujaanzishwa. Hakuna ubishi kuwa hayo ni mafanikio makubwa ya kujivunia.
Wananchi wanatakiwa kupongezwa, kwa kujitolea kwa hali na mali kuchangia ujenzi wa shule hizo hadi kufikia mafanikio yaliyopo sasa. Jitihada zao kwa kushirikiana na Serikali, zinatuhakikishia kuwa taifa la baadaye tunalolijenga sasa, litakuwa na wasomi wengi wenye mwelekeo mzuri wa kupambana na mazingira yao na kujiletea maendeleo kwa haraka.
Pamoja na mafanikio hayo, kuna jambo ambalo mara nyingi huwa natamani kulizungumzia na kwa kupitia njia hii. Nina imani kuwa ujumbe wangu, utafika kwa Rais Jakaya Kikwete na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Jambo hilo sio jingine, bali ni uimarishwaji wa elimu ya ufundi nchini. Kwangu mimi naamini kuwa elimu ya ufundi, ndio injini muhimu ya kuleta maendeleo ya haraka, kuliko kutegemea elimu ambayo inamjenga mtu kuajiriwa pekee.
Elimu hiyo ya ufundi ni muhimu zaidi, ikizingatiwa kuwa nchi nyingi ambazo zimepata maendeleo ya haraka, ziliwekeza katika elimu hiyo. Hatua hiyo ilisaidia kuzalisha wataalamu wengi, ambao kwa kutumia ujuzi na ubunifu wao, waliweza kuzalisha bidhaa ndogo ndogo, ambazo zinaendana na mahitaji husika.
Nchi kama China kwa kiwango kikubwa imewekeza katika ufundi huo. Sasa nchi hiyo ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa ndogo ndogo, ambazo zinauzwa kwa wingi katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Hivyo, kuna kila sababu kuhakikisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu inaweka mikakati ya kuboresha elimu ya ufundi nchini, kwa kujenga vyuo vya ufundi katika kila Tarafa nchini, vitakavyofundisha wahitimu wa elimu ya sekondari ili waweze kujiajiri wenyewe.
Kama kila kata nchini kwa sasa imeweza kuwa na sekondari zaidi ya mbili na zingine sekondari hadi tatu, kwa nini tushindwe kujenga chuo kimoja cha ufundi katika kila Tarafa ili visaidie kufundisha watoto wetu mara wanapomaliza elimu ya sekondari?
Hofu yangu kubwa ni kuwa wanafunzi wengi wanaomaliza kidato cha nne, hawapati nafasi ya kujiunga na kidato cha tano, hivyo kuwafanya wabaki mitaani. Hali hiyo inasababisha elimu hiyo kukosa thamani.
Lakini kwa kujenga vyuo hivyo, tutakuwa tunawahakikishia watoto wetu kuwa mara wanapomaliza elimu ya sekondari na kushindwa kuendelea na kidato cha tano, watajiunga na masomo ya ufundi moja kwa moja.
Hiyo itasaidia uchumi wa nchi kukua kwa haraka, tofauti na sasa, kwani wahitimu hao wataweza kupata stadi za kuyamudu mazingira yao na kuzalisha mali kulingana na maeneo waliyopo, badala ya kutegemea ajira, ambazo kwa sasa zimekuwa haba.
Katika kutekeleza hilo, yawezekana kutokea kwa upungufu wa wataalamu wa kufundisha katika vyuo hivyo. Lakini, najua serikali ina nchi marafiki ambazo zimepiga hatua kubwa katika teknolojia, hivyo inaweza kuomba wataalamu watakaofundisha kwenye vyuo hivyo.
Tusiogope gharama ya kupata wataalamu kutoka nchi nyingine, kwani nina imani kuwa baada ya miaka mitano au zaidi, nchi itakuwa na wataalamu wenye uwezo wa kubuni na kutengeneza vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufundisha wanafunzi katika vyuo hivyo. Kwa kuwa tumefanikiwa kutekeleza MMES, basi sasa ni vema serikali ianzishe mpango wa kujenga vyuo vya ufundi katika kila tarafa nchini.
Author:Hudson Kazonta
Daily News; Thursday,June 12, 2008 @00:05
Thursday, June 12, 2008
Subscribe to:
Posts (Atom)